![]() |
NASEEB Abdul ‘Diamond’ |
Diamond alitakiwa kufanya shoo Jumamosi iliyopita na nyomi la nguvu likatinga lakini dogo huyo hakutokea, hivyo msala kumgeukia promota.
Mashabiki walivunja vioo, viti na vitu vingine ndani ya klabu hiyo kama sehemu ya kujipoza na machungu ya kuingizwa mjini na sasa menejimenti ya Triple A inamdai promota.
Mbwana Iman aliye Mkurugenzi wa Arbab MD Entertainment, aliiambia Showbiz kuwa alishakubaliana vizuri na Diamond, akamtangulizia malipo ya awali lakini mambo yalikwenda kinyume.
“Nilimpa shilingi milioni 1.5 kama malipo ya awali. Alibaki ananidai milioni 1.5. Jumla ya malipo yote yalikuwa ni m3. Tumemsubiri mpaka jioni lakini usiku akasema amechelewa ndege. Mashabiki wamevunja vitu kwa hasira na sasa mimi nadaiwa ili nilipe,” alisema promota Mbwana.
Showbiz imebaini kuwa kutokana na tukio hilo, zipo kampeni za chini kwa chini ambazo zinafanyika ili kumpoteza Diamond, ikiwezekana asisikike kabisa kwenye redio yoyote ya Arusha.
Diamond alizungumza na Showbiz, hii ni kauli yake: “Ni kweli, wakati naelekea airport, nilikutana na foleni kali Ubungo. Nikageuza na kupita boda ya Mabibo, napo ikawa shida. Baadaye wakati foleni yetu inatembea, kwa bahati mbaya niligonga gari kwenye ukingo wa daraja. Gari likaharibika kabisa.
“Ikabidi gari niliache pale, nikakodi pikipiki niwahi airport. Kuna watu walijitahidi kunisaidia kuzuia ndege nipande lakini ikashindikana. Ikabidi nitafute ndege nyingine nikakosa, nikaenda kule Terminal 1 nipate ndege ndogo ya kukodi nikakosa. Nilihangaika mpaka saa sita.”
Jumamosi iliyopita, Showbiz ilimuona Diamond akiwa na mchumba wake, Wema Sepetu kwenye boda ya mabibo, akihangaika na foleni.
Baada ya kupata ajali, mrembo huyo ambaye ni Miss Tanzania 2006-07 ndiye aliyebaki na gari, wakati mwanamuziki huyo alikwea bodaboda kuwahi ndege.
(Imeandikwa na Joseph Ngilisho)
No comments:
Post a Comment