Chuma Blog

Katibu
Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego akisistiza jambo kuhusu haja ya
kulipamba taifa na kazi za Sanaa za nyumbani kwenye kikao cha awali cha
maandalilzi ya kampeni hiyo. Kulia kwake ni Rais wa Shirikisho la Sanaa
za Ufundi nchini Adrian Nyangamalle.

Rais
wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Bw.Nyangamalle akichangia kuhusu
mikakati ya uzinduzi wa kampeni hiyo ambayo kama ikifanikiwa
italipendezesha taifa na kazi mbalimbali za mikono.

Wajumbe waliohudhuria kikao hicho wakifuatilia mchango wa mmoja wa wajumbe kwa makini.
Na Mwandishi Wetu
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za
ufundi nchini liko mbioni kuzindua kampeni ambayo italenga kujenga
msukumo wa kulipamba taifa na Sanaa mbalimbali nyumbani.
Akizungumza
wiki hii kwenye kikao cha awali cha maandalizi ya kampeni hiyo
kilichofanyika BASATA jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa baraza
hilo Ghonche Materego alisema kuwa, lengo ni kuhakikisha maeneo ya miji,
majiji, manispaa, ofisi, mahoteli na mazingira mbalimbali yanaona
umuhimu wa kununua sanaa za nyumbani na kuzitumia kupamba.
“Hatujapamba
kabisa kwa sanaa zetu, maeneo mengi ya miji, kuta za maofisi, nyumba
zetu na kadhalika ni matupu. Ni wazi kunahitajika msukumo wa pekee
katika kuhakikisha tunaipendezesha nchi yetu kila mahali na Sanaa
mbalimbali” alisisitiza Materego.
Kwa
mujibu wa Materego, Tanzania ni nchi iliyojaaliwa vipaji vingi na yenye
historia ya pekee katika Sanaa za Ufundi hivyo ingetarajiwa sanaa hizo
kupamba kwa wingi miji, fukwe, maofisi, shule, majumba, mahoteli na
maeneo mbalimbali.
“Sasa
kama wasanii tuingalie nchi yetu, tujiweke mbele katika kuangalia namna
ya kuipamba kwa Sanaa zetu.Tukichelewa itapambwa na Sanaa za nje”
aliongeza Materego.
Alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete kwa kutilia
mkazo mapambo ya Sanaa za nyumbani na kutoa wito kwa ofisi zingine za
umma kuiga mkakati huo kwani ni aibu kutumia sanaa za nje kupamba.
“Mara
baada ya Rais Kikwete kuingia Ikulu kulifanyika ukarabati, maonesho ya
Sanaa za ufundi yaliandaliwa ili kupata Sanaa za kuipamba Ikulu yetu,
hili ni jambo la faraja kwamba, na sisi tuna pa kuanzia” alisema
Materego.
Alitaja faida za kampeni ya kulipamba taifa na Sanaa za nyumbani kuwa ni pamoja na kutanua soko la kazi za wasanii, kulipendezesha taifa na kazi mbalimbali za mikono, kuwathamini wasanii na nyingine nyingi.
Nchi
ya Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayovuma kwa Sanaa za Ufundi
duniani kama michoro, vinyago, ususi na kadhalika lakini pamoja na
utajiri huo bado Sanaa hizi hazijapewa nguvu kubwa ndani ya mipaka.
No comments:
Post a Comment