Friday, July 27, 2012

Pupa katika mapenzi inapunguza uwezo wa kufikiri

Chuma Blog


TUMEKUTANA tena katika kona yetu kujuzana machache kuhusiana na maisha yetu ya kila siku. Wote tunatambua tumo ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhan, basi niwatakie wafungaji wote Ramadhan Kareem.
Kama kawaida tunaendelea na mada zetu, nimepokea malalamiko mengi katika uhusiano, yanayotokana na mtu kupenda na kugeuzwa mtumwa wa mapenzi na kupata mateso mazito.
Kwa nini unageuka mtumwa wa mapenzi?
Wengi wamekuwa wakiteswa na mapenzi kwa vile hawakuyasoma mwanzo, matokeo yake huwa sawa na mtihani mgumu usiojua majibu yake, lazima utafeli.
Mapenzi yanasomwaje?
Wengi huyachukulia mapenzi kama starehe na kusahau kuwa ni mwanzo wa kujenga familia, tumekuwa tukiingia kwenye mapenzi kwa njia ya macho na si kutumia akili.
Nina maana gani?
Binadamu tumeumbwa na tamaa, kila kiumbe kinapenda kitu kizuri, macho huwa ya kwanza kuona na kupeleka taarifa kwenye moyo ambao nao hulipokea jambo kama lilivyo na kulitaka kwa vile ni zuri, bila kuangalia faida na hasara zake.
Hii hutokana na nini?
Siku zote pupa hupoteza uwezo wa kufikiri, hasa pale mtu anapoamini kuwa kutaka kumjua kiundani mpenzi wako ni kupoteza muda, wengi huhofia kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha umpoteze mpenzi wako na akachukuliwa na mtu mwingine.
Kila mwanadamu anatanguliza tamaa ndiyo upendo unafuata, wengi wetu huwa na pupa baada ya kumtamani mtu kwa muda mrefu. Siku ukibahatika kumpata, pupa hutangulia mbele, hivyo kufurahia bahati ile na kusahau katika mapenzi kuna kitu cha ziada.
Kweli mapenzi ni bahati nasibu lakini bado tunatakiwa kupoteza muda kidogo baada ya kumpenda mtu, lazima ujue historia yake, udhaifu wake kitu ambacho kitakusaidia kurekebisha kabla ya kuingia katika uhusiano kamili.
Wengi wetu tumeponzwa na pupa, tunakuwa kama samaki, hatufikiri, baada ya kuona chambo tunameza tu bila kujua madhara yake.
Watu wa aina hii huja kushtuka wapo ndani ya uhusiano kamili, hivyo kubakia kuteseka na kugeuka watumwa wa mapenzi, kila siku kulia na kujiona una bahati mbaya kwa kulitupa penzi lako jalalani na kukosa heshima ya mapenzi.
Siku zote mwanadamu ameumbwa akiwa na sifa kuu ya kufikiri kabla ya kutenda na anayefikiri huwa hana pupa, hufikiri kwa kituo na kupata jibu kuwa hili linafaa na hili halifai.
Hata kama uliyempata alikuwa chaguo la moyo wako, kwa vile ulitanguliza pupa, sasa hivi amegeuka chukizo la moyo wako, kila siku mateso ya upande mmoja. Kabla ya kupenda jiulize unayempenda naye anakupenda?
Utamjuaje?
Uwe mkweli na muwazi, pia kuwa tayari kuishi maisha ya aina yoyote, hamuwezi kuishi maisha ya furaha mkiwa na kitu tu na kama hakuna kitu basi kero mtindo mmoja na kuiona nyumba yako kama mochwari.
Siku zote kwa muda mfupi lazima utagundua vitu vingi kwa mpenzi unayetaka kuwa naye kama udhaifu wake ambao utaufanyia kazi kabla ya uhusiano na kama hawezi kubadilika basi hakufai, bado una kazi ya kumtafuta mwingine kwa utulivu, acha pupa.
Kwa Hisani ya:  GLOBAL

No comments:

Post a Comment