Mwanaisha Abdallah, almaarufu Nyota Ndogo alizaliwa Pwani ya Kenya yapata miongo mitatu na robo iliyopita. Mwanaisha alilelewa katika mazingira magumu. Hili lilimlazimu yeye kuambulia kufanya kazi duni ikiwemo ile ya mtumishi wa nyumbani. Ni kutokana na bidii yake ndipo alipogundua na kuamua kukitumikisha kipaji chake.
Alianza kurekodi muziki wake katika studio za Tabasamu records mjini Mombasa. Sauti yake yenye mnato na mvuto pamoja na mashairi yaliyopangika vyema ndicho kivutio kikubwa katika kazi zake. Miongono mwa kazi zake zilizomtambulisha Nyoa Ndogo ni mambo kombo. Ni kazi inayozungumzia changamoto zinazowazonga watumishi wa nyumbani.
Ukitazama video yake hii ya mambo kombo, utagundua waziwazi jinsi watumishi wa nyumbani wanavyopata matatizo wakiwa kazini. Matatizo haya anavyosema Nyota mwenyewe ni kwamba ameshayapitia. Kupigwa na dhuluma nyinginezo ni baadhi tu ya mambo yanayowakabili watumisi wa nyumbani.
Wimbo mwingine uliotia fora ni Chereko. Wimbo huu unamzungumzia msichana chiriku ambaye anakosa kusikia mawaidha na hatimaye kuambulia kuathirika kimaisha.
Baadhi ya vibao vya nyota vimempa sifa na kumpelekea kutambulika kote Afrika. Ameteuliwa na kushinda tuzo kadha likiwemo lile la Nzumari awards linaloandaliwa hapa Pwani. Vibao vyake vingine ni kama; watu na viatu, natafuta, hao, wanionea miongoni mwa vibao vingine. Nyota kwa sasa nimtangazaji katika kituo kimoja cha radio mjini Mombasa. Mwanaisha amefanikiwa kupata watoto wawili.

No comments:
Post a Comment