Thursday, November 17, 2011

UTAFITI: UMOJA WA WASANII NI TATIZO KATIKA MAENDELEO YAO

Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego akionesha kitabu kilichoandaliwa na Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, Martin Mandalu kinachohusu Tasnia ya Muziki Mkombozi Kwa Vijana kwenye Jukwa la Sanaa wiki hii. Kulia ni mtunzi huyo, Bw. Mandalu.
Na Mwandishi Wetu
Utafiti uliofanywa kwenye muziki wa kizazi kipya ukilenga kubaini changamoto na mafanikio yake umebainisha kuwa, kukosekana kwa umoja miongoni mwa Wasanii ni moja ya sababu kubwa ya kudumaa kwa maendeleo yao.
Sababu zingine zilizotajwa ni pamoja na Wasanii kutokuzingatia mikataba kwenye kazi zao, utengenezaji wa kazi za sanaa zenye ubora hafifu, usimamizi dhaifu wa kazi zao, kukosekana kwa viongozi thabiti katika tasnia ya muziki na sababu zingine.
Akiwasilisha utafiti wake alioukamilisha Mwaka huu kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii , Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, Martin Mandalu alisema kuwa, bila wasanii kuzifanyia kazi changamoto hizo bado kutakuwa na safari ndefu katika kuyafikia mafanikio ya kweli.
“Asilimia 80 ya Wasanii waliohojiwa kwenye utafiti huu hawakuwa na taarifa ya uwepo wa umoja unaowaunganisha. Hii ni hatari kwa sababu nilipofika katika vyombo rasmi nilipata taarifa za uwepo wa vyama na mashirikisho ya wasanii. Hii ina maana wasanii hawatambui uwepo wa umoja huo” alisema Mandalu.
Kwa mujibu wa utafiti huo, Wasanii wengi waliohojiwa walikiri kuwa, wamekuwa wakipata mapato kidogo ikilinganishwa na kazi wanazofanya lakini hili likielezwa kuwa linasababishwa na kutozingatia mikataba, kukosekana kwa ushirikiano miongoni mwao na Wasani kutaka kufanya kila kitu yaani utunzi wa nyimbo, usambazaji na hata umeneja.
“Wasanii wengi waliohojiwa walionekana kukosa uongozi na usimamizi thabiti. Walionekana kufanya kila kitu kuanzia utunzi wa nyimbo, kuzifanyia matangazao, kutafuta kazi za maonyesho na umeneja kwa ujumla” alisisitiza Mandalu wakati akifafanua utafiti wake.
Kuhusu utayari wa Wasanii kutoa taarifa au kufika maeneo wanayohitajika, Mhadhiri huyo msaidizi alisema kuwa, ni tatizo kubwa kwani wasanii wengi wamekuwa wazito katika hilo na hata kutokutoa ushirikiano wa kutosha katika masuala yanayowahusu.
“Wengi wa wasanii niliokuwa napanga kukutana nao, walikuwa hawaoneshi ushirikiano. Anaweza kukwambia tukutane saa tano lakini ukifika muda huo anakwambia ana kazi nyingine kwa hiyo haitawezekana” alisema Mhadhiri huyo wakati akieleza changamoto alizokumbana nazo.
Utafiti huo ambao umechapishwa kwenye Kitabu cha Tasnia ya Muziki Mkombozi kwa Vijana umefanywa na Mhadhiri huyo kama sehemu ya kupata shahada yake ya uzamili katika stadi za Maendeleo.

No comments:

Post a Comment